soundcloud

SAHAMA HAMAD 18 - Pata taarifa mbalimbali za Kisiasa, Uchumi, Dini pamoja na simulizi mbali mbali za kusikitisha zikiambatana na Makala pamoja na Tahrir za Kusisimua.. Pia tuwasiliane kupitia +255659887692 AHSANTENI...

Saturday, 11 February 2017

MWANZO MPYA UMEWADIA

Tumerejea tena kwa lengo la kukupasha habari na matukio mbalimbali kutoka ulimwenguni kaa nasi.

Friday, 23 December 2016

MAKAMU WA RAIS ATOA NENO KWA WAZAZI NA WALEZI.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka wazazi na walezi wa Tanzania Zanzibar waache tabia ya kuwaoza wasichana wa kike wakiwa na umri wadogo bali wawasomeshe kwa ajili ya manufaa yao ya jamii kwa ujumla.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti wakati akizindua madrasa ya kisasa iliyojengwa kwenye eneo la kilimani na kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa na ujenzi wa msikiti mkubwa kuliko yote nchini Tanzania unaojengwa katika eneo la Ijitimai kidoti katika Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa michango ya wananchi katika siku yake ya kwanza ya ziara ya Kikazi Kisiwani Unguja.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kama wazazi na walezi watasomesha watoto wa kike elimu watakayopata itasaidia kwa kiasi kikubwa wasichana hao kufanya maamuzi sahihi na yenye tija katika jamii.

Amesisitiza kuwa pamoja na elimu kuwa ni haki ya msingi kwa mtoto wa kike hivyo ni muhimu kwa jamii nzima ya Zanzibar ihakikishe watoto wa kike wote wanapata elimu kwani watakuwa na uwezo wa kuchagua na kuandaa mustakbali wa maisha yao ya baadaye ikilinganishwa na hali ilivyo sasa kwenye baadhi ya maeneo.

Kuhusu elimu ya dini, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewahimiza wazazi na walezi kuwalea watoto katika maadili mema kwa kuzingatia maandiko matakatifu ya Mtume Mohammad (S.A.W).

Amesema vijana wengi wanaolelewa kwa kufuata misingi ya bora ya dini ni vigumu kurubuniwa na kujiingiza katika matendo yasiyofaa katika jamii.

Wednesday, 8 June 2016

#KESHI HATUNAE TENA DUNIANI.

KESHI HATUNAYE TENA DUNIANI.
Nigeria. Nahodha na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Nigeria Stephen Keshi (54) amefariki dunia mapema leo jijini Benin katika jimbo la Edo State.

Msiba huu umekuja ikiwa ni mwaka mmoja umepita tangu mwanasoka huyo ampoteze mkewe, Kate Keshi, baada ya kuugua saratani kwa muda mrefu.

Keshi atakumbukwa kuwa miongoni mwa wanasoka wa kipekee kabisa nchini Nigeria kwani amewahi kutwaa kombe la Mataifa ya Afrika akiwa mchezaji na kama kocha wa kikosi cha Super Eagle.

“Keshi hakuwa mgonjwa kabisa, hajawahi kuonyesha dalili zozote za ugonjwa, lakini tunahisi kifo kimesababishwa na msongo wa mawazo mara baada ya kifo cha mkewe,” mmoja wa marafiki wa Keshi ameliambia TheCable.

Keshi alizaliwa Januari 23, 1962 huko Azare katika jimbo la Bauchi na kuanzia soka lake katika timu ya ACB Football Club, baadaye akajiunga na klabu za New Nigeria Bank, Stade d’Abidjan, Africa Sports, Lokeren, Anderlecht na RC Strasbourg.

Tuesday, 24 May 2016

#MSHAURI WA UCHUMI:

Rais Dkt.John Pombe Magufuli amemteua Profesa Longinus Rutasitara kuwa Mshauri wake katika masuala ya Uchumi.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Rais Ikulu, Dar es Salaam ikimnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi ilieleza kuwa uteuzi huo unaanza mara moja,Profesa Rutasitara alikuwa Mhadhiri wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

#Maalimu seif kuhojiwa na jeshi la polisi Zanzibar.


Jeshi la Polisi Zanzibar litamhoji Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad Ijumaa ya wiki hii kuhusu masuala mbalimbali ambayo hata hivyo, hayakuwekwa wazi.

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdani Makame alisema jana: “Natambua kuwa wasaidizi wangu watazungumza naye Ijumaa. Wao ndiyo wanajua watamhoji nini.”

Alipoulizwa kuhusu mahojiano hayo, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Salum Msangi naye hakuweka wazi badala yake alisema kuna masuala mengi ambayo ofisi yake inahitaji kuyafahamu kutoka kwa Maalim Seif.

Hii ni mara ya kwanza kwa Maalim Seif kuhojiwa na polisi tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu ambao kwa Zanzibar ulirejewa Machi 20, baada ya ule wa Oktoba 25 mwaka jana kufutwa.

Maalim Seif ambaye kabla ya uchaguzi huo alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alipinga kurudiwa kwa uchaguzi huo msimamo ambao pia ulichukuliwa na chama chake.

Kiongozi huyo amekuwa akitoa matamko kadhaa ya kuwashawishi wananchi kupinga utawala wa Serikali iliyopo madarakani.

Akiwahutubia wafuasi wake huko Pemba hivi karibuni, Maalim Seif alisema Serikali ya CCM imeanza kutikisika kutokana na vikwazo vinavyoendelea kuwekwa na wahisani pamoja na hatua ya chama chake CUF kutowatambua viongozi wake pamoja na Serikali. 

“CCM wajue wamekalia kuti kavu, siku yoyote wataanguka... tufanye kazi mpaka haki yetu tuhakikishe imerudi na wenzetu hawana safari ya kudumu,” alisema.

Aliwataka wanachama wake kuonyesha kwa vitendo kutoitambua Serikali ikiwamo kukataa kulipishwa kodi za ovyovyo pamoja na kujitenga na viongozi wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Mfano tunaweza kuamua siku fulani kuanzia saa sita, tunasimamisha vyombo vyote vya usafiri na siku nyingine tunaamua kupiga honi Zanzibar nzima kuonyesha hatuitaki Serikali ya CCM,” alisema huku akishangiliwa na umati uliofurika katika ofisi za chama hicho.

Mapema jana, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo alisema kuwa amesikia juu ya wito huo lakini hakuwa amepata taarifa rasmi kutoka kwa mkuu wake.

“Nimesikia kama mlivyosikia ninyi,” alisema na kuongeza: “Nimeelezwa pia hata leo Kamishna wa Polisi Zanzibar alikuwa na mahojiano naye.”

Kuhusu hilo Kamishna Makame alisema:“Sijaonana wala kuzungumza naye leo. Hiyo si kweli.”

Juzi, wakati akizindua ripoti ya Uvunjifu wa Haki za Binadamu uliofanyika visiwani humo kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema wanazo taarifa za Serikali kutaka kuwakamata viongozi waandamizi wa chama hicho na kuwashikilia.

Alisema wamebaini mpango wa kukamatwa kwao na kuwekwa kwenye Mahakama za bara ili kuwanyamazisha Wazanzibari.

Tuesday, 22 March 2016

#ZANZIBAR YA MWAKA 2010 IPO WAPI?

#ZANZIBAR YA MWAKA 2010 IPO WAPI?
Visiwa vya Zanzibar ni visiwa ambavyo Allah amevijalia neema nyingi ambazo hupatikana katika visiwa hiyo mimea ya kila aina yenye kustawi ardhi, ubluu wa bahari yenye kila aina ya neema,  jamii ya Watu walio na ustaarabu na busara na vingi vyenginevyo pamoja na kujalia zao kubwa la kibiashara la karafuu lenye kuingiza pato kubwa la mapato, vivutio vya kila aina ambavyo huwafanya watali kujaa katika visiwa hivyo kila mwaka.

Vitu hivyo vyote pamoja na vyengine vingi huaribiwa na chuki za kisiasa, zinazosababisha na baadhi ya Watu wenye kujali maslahi ya matumbo yao na kuwacha ukaribmu, busara walizokuwa nazo Watu wa visiwa hivyo vya Unguja na Pemba.

Tunafahamu ya kuwa siasa za uhasama zilianza kipindi kirefu visiwani humo tokea pale mfumo wa vyama vingi ulipoanza na kuendelea kwa miaka kadhaa.

Lakini ahuweni tuliipata pale viongozi wazalendo wa taifa hilo walipotoa tofauti zao za kisiasa na kuangalia Zanzibar yao kwanza na kufanikiwa kuondoa chuki na uhasama walizokuwa nazo wananchi wa visiwa hivyo.

Ukweli usiofichika Dr amani abeid amani karume aliyekuwa rais wa Zanzibar kati ya mwaka (2000-2010) na katibu mkuu wa Cuf maalim seif Sharif hamad walionesha uzalendo wao kwa kuwaleta wananchi wa visiwa hivyo kuwa wamoja na kufanikiwa kuwaondoa katika misingi ya chuki,uhasama, na ubaguzi wa uunguja na upemba waliokuwa nao wakazi wa visiwa hivyo.

Viongozi hao walifanya kazi kubwa ya kuwaunganisha wazanzibar na kuhakikisha wanawafanya wazanzibar waweze kupendana na kuthaminiana na kujiona kwamba wao ni wamoja.

Ukweli ulidhihirika katika uchaguzi uliofuta wa mwaka 2010 kuanzia kwenye kampeni za uchaguzi huu mpaka pale matokeo ya urais yalipotangazwa ambapo tuliona upendo waliokuwa nao wazanzibar kwa kuondoa uccm na ucuf waliokuwa nao na kuweka uzanzibar kwanza.

#INAENDELEA

Saturday, 19 March 2016

#TAMKO LA UMOJA WA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA

TAMKO LA UMOJA WA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA JUU YA KUTEKWA KWA MWANDISHI WA HABARI WA SAUTI YA UJERUMANI ( DW ) SALMA SAID.

Salma Said mwandishi wa DW Zanzibar ametoweka baada ya kutekwa na watu ambao hawajafahamika jijini Dar es salaam, hali ambayo imeleta fadhaa na mshtuko kwa waandishi, jamii na familia yake hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa marejeo Zanzibar.

Ifahamike kuwa Kazi ya mwandishi wa habari ni kutoa habari juu ya kila kinachoendelea katika jamii , hivyo kama kuna dosari , dosari hiyo ni ya jamii na sio ya anayeieleza dosari .

UTPC inalaani na kupinga utekaji uliofanywa ambao sababu zake bado hazijulikani, hivyo tunaitaka serikali kuhakikisha Salma Said anatafutwa, kupatikana na anaachiwa huru mara moja kwa kuwa Serikali ndio yenye jukumu la kulinda raia wake.

Kama utekwaji wa Salma umefanywa kutokana na kazi yake ya uandishi habari tunalaani vikali hatua hiyo, vitendo hivi havipaswi kuendelea katika nchi inayoheshimu misingi haki na Demokrasia, Vitendo vya namna hii vinadumaza na kufifisha uhuru wa habari .
Tunapinga kwa nguvu zetu zote waandishi wa habari kukamatwa na vyombo vya dola au makundi ya kihalifu kwa visingizio ama vya uchochezi au maslahi ya taifa.

Waandishi tutaendelea kufanya kazi zetu bila kujali vitisho vya aina yoyote ile kutoka kwa mtu yoyote au Serikali.
Imetolewa na

DEOGRATIUS NSOKOLO
RAIS WA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA -UTPC.
March 19, 2016.