Jioni ya tarehe 29 Machi 2015, msafara wa wafuasi wa Chama cha Wananchi
(CUF) waliokuwa wakitoka Makunduchi, kusini Unguja, kuelekea Mjini
Magharibi, ulishambuliwa njiani na ‘watu wasiojulikana.’ Hilo neno ‘watu
wasiojuilikana’ tuliwache hivyo hivyo kwenye alama za mashaka, maana ni
mtazamo wangu kwamba ni kinyume chake, yaani ni ‘watu wanaojuilikana’
na wale wanaopaswa na wenye wajibu wa ‘kujuwa’ mambo kama haya.
Kwa mujibu wa mmoja wa watu waliokuwamo kwenye msafara huo “gari ya
‘majanjawidi’ ikiwa katika mwendo wa kasi iliupita msafara wao na kisha
kuwarushia watu waliokuwemo katika gari hiyo visu na nondo.” Muda
mchache uliopita, Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim
Seif Sharif Hamad, alikuwa amewaomba watu wote walioshiriki mkutano huo
huko Makunduchi, waondoke kwenye msafara mmoja kurudi mjini.
Inaonekana
alishakuwa na wasiwasi juu ya kile ambacho kingelitokea na ushauri wake
ulilenga, yumkini, kukizuwia kisitokee.
Siku tano kabla ya hapo, ofisi za CUF jimbo la Dimani, mkoa wa Mjini
Magharibi, zikateketezwa kwa moto na ‘watu wasiojuilikana’ na
kusababisha hasara kubwa. Mashuhuda wa tukio hilo, ambalo lilitokea mtaa
wa Kisauni saa 8: 00 usiku, wanasema watu hao walifika na gari aina ya
Pick-up na kuvunja mlango wa ofisi hizo na kuliripua jengo hilo kwa
petroli. Kwa mujibu wa Diwani wa wadi ya Tomondo, Hassan Hussen Yussuf,
jengo hilo lilikuwa na vifaa mbalimbali vya thamani na fedha taslimu za
malipo ya uchukuaji wa fomu za wagombea walizolipia.
Kuchomwa kwa ofisi za CUF Dimani kulikuja siku tatu tu baada ya chama
hicho kufanya mkutano kwenye eneo la jirani na hapo kwa kile
kilichosema ni “kumgotoa” Mansoor Yussuf Himid, ambaye anarudi kugombea
uwakilishi kwa tiketi ya CUF katika jimbo la Kiembesamaki. Mansoor
alikuwa mwakilishi wa jimbo hilo hapo kabla kwa tiketi ya Chama cha
Mapinduzi (CCM), kabla ya kufukuzwa kutokana na msimamo wake kuelekea
Muungano wa Tanzania na nafasi ya Zanzibar kwenye Muungano huo. Kwenye
mkutano huo kulizungumziwa kuwepo kwa njama za kuiingiza Zanzibar katika
machafuko kabla ya kura ya maoni ya Aprili 30 mwaka huu na kuelekea
uchaguzi mkuu wa Oktoba 25. Wito wa wazungumzaji wa CUF kwenye mkutano
huo ilikuwa “kutochokozeka” na “kutoondoshwa kwenye mstari.”
Mkutano huo nao ulitanguliwa na mkutano wa wazee wa CUF kwenye ukumbi
wa Salama, Hoteli ya Bwawani Zanzibar, ambako pamoja na mengine mengi,
Maalim Seif naye alizungumzia mipango hiyo ya fujo zinazopangwa na
zilizokwishafanywa huko nyuma. Na yeye akasogea mbele zaidi kwa
kurejelea tamko la “kutofukua makaburi” lau chama chake kitachukuwa
madaraka kamili baada ya uchaguzi wa Oktoba. Kwa hakika, aliwakemea wote
waliomo kwenye chama chake, ambao wanadhani kwamba ikiwa CUF itaingia
madarakani, itakuwa zamu yao ya “kutesa.”
Mstari wa makala hii unapigwa hapa ambapo nadhani pana haja ya
kushereheshwa na sio kutafsiriwa tu. Kusherehesha – kwa wasioufahamu
vyema msamiati huu na asili yake – kuna maana ya kuchambua tafsiri,
wakati kutafsiri ni kuhamisha maana kutoka chanzo kimoja kupeleka
chengine. Asili ya neno kusherehesha ni kwenye madarasa ya dini, ambako
masheikh wanaotafsiri Qur’an huchambuwa maana ya kile walichokitafsiri
kwa upana na marefu.
Kwa maoni yangu, kauli za “kutochokozeka”, “kutoondoka kwenye
mstari”, “kutokufufua makaburi” na “kutolipiza kisasi” ni za muhimu sana
katika kujenga siasa za Maridhiano visiwani Zanzibar na kulivuta kundi
ambalo hadi sasa linayapinga Maridhiano hayo kwa kuwa tu lina wasiwasi
juu ya hatima yake, endapo CUF itaingia madarakani. Lakini kwa umuhimu
huo huo pia, panahitajika kuchorwa mstari na kuwekwa vituo ili kundi
lililokwishaamua kuiangamiza Zanzibar, liujuwe pia ulipo mpaka kati ya
kile wenzao wanachokichukulia kuwa ni uvumilivu lakini wao wakakiona ni
ubwege.
Kwa namna yoyote ile, sidhani ikiwa CUF inakusudia kulipa kundi hilo
la ‘watu wasiojuilikana’ hundi safi mkononi mwao ili liijaze litakavyo,
kisha liondoke zake bila kuguswa. Sidhani hivyo, maana huko ni kwenda
kinyume na hata misingi mikuu ya kuundwa kwa CUF yenyewe, ambayo ni haki
za binaadamu na utawala wa sheria. CUF haivuni chochote kwa
kuwapunguzia khofu watu hawa zaidi ya kuwahakikishia kile kinachoitwa
‘impunity’, yaani uwezo wa kukwepa sheria. Wanachofahamu wao pale
wakiambiwa kwamba “makaburi hayatafukuliwa” ni kuwa wamepewa ruhusa ya
kuendelea kupiga, kujeruhi na hata kuua, wakijuwa kuwa hatimaye hakuna
mahakama wala jela inayowasubiri. Huo ndio uzoefu wao, maana hawajaanza
leo wala jana kuyafanya haya.
Akili ile ile ya kutia moto mabanda ya skuli na vinyesi kwenye
visima, ndiyo akili ile ile iliyounda Melody, kisha ikaja na Janjawidi
na Mbwa Wakali na Ubaya Ubaya. Madhara yale yale ya miaka ya ’90, ndiyo
yaliyokuwa ya 2000, 2005 na sasa 2015. Kundi hili, lenye akili hizi,
halihitaji kuambiwa kuwa makaburi yake hayatafukuliwa, ikiwa bado
linaendelea kuyatenda yale yale. Makaburi yao yanapaswa kufukuliwa na
maovu yao kuanikwa hadharani na, zaidi kuliko yote, kufikishwa kwenye
vyombo vya sheria.
Zanzibar ijayo baada ya Oktoba 2015 inapaswa kuwa ya kuvumuliana na
kushirikiana kuijenga kiuchumi, kijamii na kisiasa, lakini hilo
halipaswi kuwapa watu nafasi mwanya wa kuichafua salama ya Wazanzibari
hivi sasa, kisha wakategemea msamaha na kuvumiliwa baadaye.
Kwa hivyo, ingawa ni sahihi kabisa kujenga moyo wa Maridhiano na
kuondosheana wasiwasi kwa wale waliotenda uovu katika zama za ujahili,
si sahihi hata kidogo kuwajengea imani waovu wa zama za leo – ambazo ni
zama za nuru. Hawa ni akina Abu Jahl. Hakuna chochote
kitakachowabadilisha na kuwafanya waikumbatie salama ya Wazanzibari
wote. Hawa lazima waelezwe kinagaubaga kuwa kuna mahakama, kuna jela, na
kuna adhabu.
Wakati tunajitahidi kuwazuwia vijana wetu wasipande jazba na kuingia
kwenye machafuko, kwani nako pia kutakuwa kwa faida ya kundi hilo la
‘watu wasiojuilikana’, tunapaswa kuchora mstari na kuweka alama zetu.
Makala ya Mohammed Ghassani kwenye zanzibardaima.wordpress.com
No comments:
Post a Comment