soundcloud

SAHAMA HAMAD 18 - Pata taarifa mbalimbali za Kisiasa, Uchumi, Dini pamoja na simulizi mbali mbali za kusikitisha zikiambatana na Makala pamoja na Tahrir za Kusisimua.. Pia tuwasiliane kupitia +255659887692 AHSANTENI...

Wednesday, 1 April 2015

mwisho wa ulaya kukomeshwa kuzingirwa ghaza


Kwa mara nyingine tena, mwakilishi wa Umoja wa Ulaya katika Umoja wa Mataifa ameutaka utawala wa Kizayuni wa Israel uache kuuzingira Ukanda wa Ghaza.

John Gatt-Rutter ametoa mwito huo katika kongamano la kamati ya kuchunguza haki za wazi za wananchi wa Palestina katika ardhi zilizotekwa na kukaliwa kwa mabavu na Wazayuni mwaka 1967.

Aidha amesema, kuna udharura kwa Umoja wa Ulaya kulisaidia taifa la Palestina hususan wakazi wa Ukanda wa Ghaza ambao wanaendelea kuteseka na madhara ya jinai za hivi karibuni za Israel. Amesema hivi sasa zaidi ya familia 30 elfu za Kipalestina zinaishi katika umaskini wa kupindukia kutokana na jinai za Israel.

 Mjumbe huyo wa Umoja wa Ulaya katika Umoja wa Mataifa amegusia pia mchango wa EU katika kudhamini bajeti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) na kuwadhaminia nafasi za kazi wakimbizi wa Palestina akisema kwamba mchango huo unafikia Euro milioni 80 kila mwaka, na ametaka Umoja wa Ulaya ufanye kila uwezalo kuhakikisha kuwa njia za kuingia na kutoka Ukanda wa Ghaza zinafunguliwa ili  kukomesha mateso waliyo nayo wakazi wa ukanda huo.

Utawala wa Kizayuni wa Israel ulianza kuuzingira Ukanda wa Ghaza tangu miaka minane iliyopita.
Kivuko cha Rafah nacho ambacho ni njia muhimu mno ya kuingia na kutoka Ghaza kimekuwa kikifungwa mara kwa mara na kwa muda mrefu na pia kuna unyanyasaji mkubwa wanaofanyiwa Wapalestina hata katika hizo mara chache wanazoruhusiwa na Misri kutumia kivuko hicho.

Hii ni katika hali ambayo zaidi ya Wapalestina 2000 waliuawa shahidi na maelfu ya wengine kujeruhiwa katika mashambulizi ya siku 50 ya Israel yaliyoanza mwezi Julai mwaka jana na hadi hivi sasa jinai za vita hivyo zinaendelea kuwatesa wakazi wa Ghaza waliozingirwa kila upande.

Katika msimu wa baridi kali uliopita, theluji ilinyesha kwa wingi sana katika Ukanda wa Ghaza huku maelfu ya wakazi wa eneo hilo wakilazimika kuvumilia baridi kala kutokana na makazi yao kuharibiwa vibaya na mashambulizi ya Israel.

 Katika vita vitatu vilivyofanywa na Israel dhidi ya Ghaza, mara zote jeshi la utawala wa Kizayuni limekuwa likilenga maeneo nyeti na muhimu kama vile vinu vya umeme, maeneo ya usambazaji maji safi, mahospitali, shule na kadhalika ili kuwashinikiza wananchi Waislamu wa ukanda huo waachane na muqawama wa kupambana kiume na jinai za Wazayuni. Hadi hivi sasa pia na licha ya kuweko mateso yote hayo, bado jeshi la utawala wa Kizayuni linafanya mashambulizi ya hapa na pale dhidi ya wakazi wa ukanda huo.

 Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kuutaka kwa maneno tu utawala wa Kizayuni uache kuizingira Ghaza hakutoshi, bali Umoja wa Ulaya unatakiwa uchukue hatua za kivitendo za kuilazimisha Israel ikomeshe jinai hizo na hasa kwa kuzingatia kuwa hii si mara ya kwanza kwa Umoja wa Ulaya kuutaka utawala wa Kizayuni uache kuizingira Ghaza lakini utawala huo katili unaendelea kufanya ukaidi.

 Umoja wa Mataifa nao unapaswa kulaumiwa zaidi kutokana na kunyamazia kimya jinai wanazofanyiwa hasa watoto wadogo huko Palestina, jambo ambalo linakwamisha juhudi za wanaharakati wa haki za binadamu za kufikisha kwa walimwengu kilio cha Wapalestina wanaodhulumiwa kwa kila namna na utawala wa Kizayuni wa Israel.