
Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, Allamah Muhammad Iqbal Lahori mwanafikra, mwanafalsafa na malenga wa Kiislamu aliaga dunia huko Bara Hindi. Alizaliwa mwaka 1873 katika mji wa Sialkot kwenye jimbo la Punjab. Baada ya kumaliza masomo ya awali na ya juu na kupata shahada ya uzamili, Allamah Muhammad Iqbal Lahori alielekea nchini Ujerumani na baadaye Uingereza kwa lengo la kujiendeleza katika elimu ya falsafa na kubaki huko kwa kipindi cha miaka minne. Malenga huyo alianza kutunga mashairi akiwa katika masomo yake ya sekondari. Baada ya kurejea India, Iqbal Lahori alianza kuwaamsha Waislamu wa nchi hiyo na kufanya jitihada za kuwaunganisha pamoja huku akibainisha fikra na mitazamo yake kupitia beti za mashairi. Mwanafalsafa huyo anahesabiwa kuwa mmoja wa waanzilishi na waasisi wa Pakistan huru.
Siku kama ya leo miaka 996 iliyopita alifariki dunia Abu Raihan Biruni msomi, mnajimu na mwanahisabati mkubwa wa Kiirani huko katika mji wa Ghazne katikati mwa Afghnaistan ya sasa. Abu Raihan Biruni alikuwa hodari katika elimu za historia, jiografia na hisabati, tiba na utengenezaji wa dawa. Akiwa safarini nchini India, msomi huyo wa Kiirani alikutana na kufanya mazungumzo na maulama na watawala wa zama hizo. Abu Raihan alikusanya taarifa muhimu alizokuwa akihitajia kwa ajili ya kuandika kitabu chake alichokiita 'Tahqiq Ma Lilhind' baada ya kujifunza lugha ya Sanskriti yaani lugha ya Kihindi ya kale.
Katika kitabu hicho, Abu Raihan ameandika taarifa muhimu kuhusu sayansi, itikadi, mila na desturi za Wahindi. Msomi huyo wa Kiirani ameandika vitabu vingine vingi kuhusu elimu ya nujumu, mantiki na falsafa.
Miaka 1186 iliyopita, Egbert Mfalme wa kwanza wa Uingereza aliingia madarakani baada ya vita vya muda mrefu. Kabla ya hapo Uingereza ilikuwa ikiendeshwa kwa utawala wa kijadi na ilikuwa imegawanywa katika sehemu kadhaa huku kila mtawala akitawala eneo lake. Egbert alikuwa mfalme wa ardhi ya Wessex na baada ya kupigana vita na watawala wa kijadi na kuwalazimisha wamtii, alichukua madaraka akiwa Mfalme wa Kwanza wa Uingereza na kuasisi utawala wa Wasaxoni. Mtawala huyo alijulikana pia kwa jina la Egbert the Saxon.
Na miaka 35 iliyopita aliaga dunia Sohrab Sepehri malenga na mchoraji mashuhuri wa Kiirani. Sohrab alizaliwa mwaka 1307 Hijria Shamsiya katika mji wa Kashan katikati mwa Iran. Awali malenga huyo wa Kiirani alianza kufundisha na baada ya hapo alijiunga na taaluma ya sanaa. Vilevile alikuwa na kipaji kikubwa katika masuala ya uchoraji. Kazi za malenga na mchoraji huyo wa Kiirani zilimpatia tuzo na zawadi nyingi katika maonyesho mbalimbali yaliyofanyika ndani na nje ya Iran. Shairi lake la kwanza alilitunga mwaka 1330 Hijria Shamsiya na kulipa jina la The Death of Colours.
No comments:
Post a Comment